Blogger Widgets

Monday, July 1, 2013

UPDATES: Je wajua Rais mstaafu wa Marekani, George W. Bush naye yupo Tanzania??


Rais Barack Obama amewasili jijini Dar es Salaam mapema leo kuhitimisha ziara yake barani Afrika na wakati akiwa hapa anatarajiwa kukaribishwa na sura anayoifahamu.
Rais aliyemtangulia, George W. Bush pia atakuwa hapa nchini kuhutubia mkutano wa Wanawake wa Afrika, na marais hao wawili wamepanga kukutana kwenye Ubalozi wa Marekani mjini Dar es Salaam kesho.
Obama na Bush wataweka mashada ya maua kukumbukia mlipuko wa bomu kwenye ubalozi huo ambao uliua watu 11 mwaka 1998.
Rais huyo wa sasa alikwenda Afrika Kusini baada ya kwanza kutembelea Senegal katika safari ya kuimarisha mshikamano wa demokrasia kati ya Marekani na Afrika.
Amepanga kukutana na Rais Jakaya Kikwete, na pia wafanyabiashara kadhaa wa Marekani na Afrika kwa matumaini ya kuimarisha biashara katika bara hilo.
Kesho asubuhi atakutana na Bush kwenye ubalozi huo kabla ya kuhutubia kuhusu nishati ya umeme barani Afrika, na kisha ataondoka kurejea Washington.
Kwa upande wake, Bush anahudhuria mkutano ulioandaliwa na Taasisi ya George W. Bush.
Wake na marais hao wawili, Michelle Obama na Laura Bush, watajumuika kwenye mkutano huo kwa majadiliano kuhusu kusaidia elimu kwa wanawake, afya na ajira.
Bush amejikita zaidi kwenye kazi yake ya kujitolea kuhusu Afrika tangu aachie madaraka ya urais, na anakumbukwa mno katika bara hili kwa kazi yake wakati alipokuwa Rais.


Reported by >>> Walee