Arusha. Serikali inakusudia kupunguza au kuondoa kabisa kodi katika ving’amuzi ili kuwezesha Watanzania wengi kumudu kununua vifaa hivyo na kupata huduma ya matangazo ya runinga.
Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba alisema jana kuwa kwa sababu Serikali inatekeleza makubaliano ya kimataifa ya kuhamia mfumo wa dijitali kutoka analojia, ni vyema kila Mtanzania akawa na uhakika wa kupata huduma ya matangazo ya runinga na hilo haliwezi kufanikiwa iwapo bei ya ving’amuzi itaendelea kuwa juu.
Akizungumza kwenye mkutano wa 21 wa Umoja wa Taasisi za Utangazaji Kusini mwa Afrika (Saba), Makamba alisema hivi sasa wizara yake inawasiliana na Wizara ya Fedha pamoja na wadau wengine kuangalia njia bora na sahihi ya kufanikisha lengo hilo.
“Tayari serikali imepunguza viwango vya kodi kwenye ving’amuzi ili kuwapa nafuu wananchi, lakini tunafikiria kuipunguza zaidi au kuondoa kabisa kodi ili kuwezesha Watanzania wote wenye seti za televisheni kupata matangazo ya runinga,” alisema Makamba.
Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, Profesa John Mkoma alisema Tanzania inajivunia kufanikiwa kutekeleza malengo ya kimataifa ya kuhamia mfumo wa dijitali kutoka analojia kulinganisha na nchi zingine za SADC.
Alisema matumizi ya king’amuzi imerahisisha gharama za matangazo ambapo hivi sasa mtu anaweza kurekodi kipindi na kukipeleka kwenye kituo cha Tv au redio kwa ajili ya kurushwa hewani.
Profesa Mkoma alisema matumizi ya dijitali pia yameboresha usikivu wa sauti na muonekano wa picha kwenye vituo vya televisheni nchini.
Tanzania ilianza kuingia kwenye mfumo wa dijitali kwa kuzima mitambo ya analojia kuanzia mwishoni mwa mwaka jana kwa kuanzia na mkoa wa Dar es Salaam mpango ulioendelea kwa mikoa mingine ya Tanzania.
Tayari baadhi ya mataifa ya Afrika Mashariki yameanza kufuata hatua hiyo ya Tanzania.