SIKU chache baada ya Waziri wa zamani na Mbunge wa Urambo Magharibi, Profesa Juma Kapuya (CCM) kutuhumiwa kumbaka na kutishia kumuua binti mdogo wa miaka 16, kiongozi huyo ameibuka na kutoa utetezi wa kujikanganya.
Akizungumza kupitia kwa wakili wake, Yasin Memba, mbunge huyo alitishia kuliburuza gazeti hili mahakamani endapo halitamwomba msamaha ndani ya siku saba.
Pamoja na kukataa kwake kumfahamu binti huyo, Kapuya amekiri kumiliki simu namba 0784993930 ambayo imekuwa ikitumiwa kuwasiliana naye ikiwemo kumtumia ujumbe mfupi wa maneno (sms) wa vitisho.
Hata hivyo, katika namna ya kushangaza, Kapuya alidai kwamba simu hiyo aliishaigawa miezi sita iliyopita, na hivyo hausiki kwa namna moja ama nyingine na tuhuma alizopewa.
Lakini wakati Kapuya akikwepa mtego huo, Novemba 9, mwaka huu, gazeti hili liliwasiliana naye kupitia namba hiyo hiyo anayodai kwamba alishaigawa miezi sita iliyopita.
Tarehe hiyo, gazeti hili liliwasiliana na mbunge huyo ili kuthibitisha tuhuma zilizokuwa zikimkabili wilayani Kaliua za kumpiga makofi kiongozi mmoja wa CCM.
Kapuya kupitia namba hiyo, alitoa utetezi wake ambapo gazeti hili lina sauti yake.
Utetezi wake pia unaongeza utata kwani hakufafanua ilikuwaje akagawa namba ya simu iliyosajiliwa kwa jina lake kwa mtu mwingine, huku ikiendelea kutuma fedha na vitisho kwa binti huyo.Katika utetezi wake jana, Kapuya alikana kutomjua binti huyo wala dada yake, na kwamba yeye si mwathirika wa ugonjwa wa ukimwi.
Alilishutumu gazeti hili kuwa lilijifanya hakimu kwa kuchapisha tuhuma zake bila kumpa nafasi ya kujitetea kama ilivyo kawaida kwenye tasnia ya habari.
Hata hiyo, ukweli ni kwamba nafasi hiyo aliipata, lakini hakuitumia kwani alipopigiwa, simu yake ilipokelewa na mtu aliyejitambulisha kuwa ni dereva wake na kutaka aelezwe sababu za kutafutwa bosi wake.
Hata alipoelezwa kuwa anayehitajika ni bosi wake, alisita kisha alitoa namba nyingine ya simu akitaka atafutwe kupitia namba hiyo.
Lakini muda wote namba hiyo haikupokelewa na hata alipopigwa tena namba ya awali, nayo iliita bila kupokelewa.
Wakili Memba alidai kuwa mteja wake, alimweleza kuwa habari ile imemletea madhara na usumbufu mkubwa katika familia yake, jamii na kumvunjia heshima yake.
"Kwa sababu hiyo, amenielekeza niwapatie siku saba gazeti la Tanzania Daima, mitandao ya kijamii ukiwemo wa Jamii Forum, Justina John na Vituko Mtaani ambao walichapisha habari hiyo, waombe radhi kwa uzito ule ule la sivyo atavishitaki mahakamani.
"Kama hawataomba radhi, basi atafungua kesi mbili, moja ni kwa ajili ya gazeti la Tanzania Daima na hiyo mitandao ya kijamii, na kesi ya pili ni ya kuhusu huyo mtoto anayedaiwa kubakwa na kuambukizwa ukimwi," alisema.
Aliongeza kuwa wanataka mtoto huyo aje mahakamani athibitishe aliambukizwaje ukimwi na alete ushahidi unaoonyesha Kapuya ana ukimwi.
Memba aliuomba umma kuelewa kuwa habari hiyo iliyochapishwa na Tanzania Daima haiusiani na chama chake wala serikali.
Kwa siku mbili mfululizo gazeti hili lilifichua tuhuma za Kapuya kudaiwa kumbaka mtoto huyo, na hata baada ya kubaini siri hiyo imevuja, alimpigia simu mtoto huyo, na baadaye kutuma meseji kadhaa za vitisho.
Tanzania Daima ilishuhudia baadhi ya meseji za simu zilizotumwa na Prof. Kapuya kwenda kwa mtoto huyo.Juzi alfajiri saa 11:21 kupitia simu yake alituma ujumbe kwa mtoto huyo: "Chagueni kunisubiri tuje tuongee au mnataka kufa?"
Baadaye saa 1:07 asubuhi, alituma ujumbe mwingine kutoka simu hiyo hiyo kwenda kwa mtoto huyo, ukisema: "Mkiuawa, itakuwa nzuri, itawapunguzia gharama za kuishi. Usitake kugombana na serikali, mtoto mdogo kama wewe. Sisi ndo wenye nchi yetu."
Baadhi ya mashirika yanayotetea makundi kadhaa yakiwamo Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na Mtandao wa Kijinsia Tanzania (TGNP) yalijitokeza kuwasaidia watoto hao, ambao ni yatima.
Mtoto huyo na dada yake, wakizungumza na gazeti hili kwa hofu mafichoni, walisema kwa sasa hawana imani tena kama kuna serikali nchini Tanzania kwa kuwa wamedhalilishwa, wametembezwa hadi bungeni na wabunge bila hatua kuchukuliwa, licha ya kutoa taarifa katika Kituo Cha polisi Oysterbay tangu mwaka jana.
Hata hivyo, kabla ya tukio la watoto hao kuripotiwa ofisi za gazeti hili, juzi usiku kulikuwa na watu waliokuja wakiwatafuta watoto hao, huku wakiwatisha kwa simu na kuwatolea maneno ya kejeli, wakidai watawamwagia tindikali.
Juzi gazeti hili lilichapisha habari kuhusu mwanafunzi huyo aliyesema kuwa waziri huyo alimbaka kwenye hoteli moja ya kitalii iliyoko jijini Dar es Salaam mwaka 2011, na kurudia tena kitendo hicho katika Jengo la Biashara Complex lililoko Mwananyamala Juni 3, 2012 alipoitwa kwenda kuchukua ada kwa mara ya pili.
SOURCE: TANZANIA DAIMA
Saturday, November 16, 2013
Prof. Kapuya atishia kuishitaki JamiiForums...!
4:18 PM