Blogger Widgets

Thursday, September 3, 2015

SIRI, HOTUBA YA DK. SLAA..

Hotuba ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Wilbrod Slaa, imepondwa vikali na wasomi mbalimbali wasiofungamana na upande wowote kisiasa.
Juzi Dk. Slaa baada ya kukaa kimya kwa muda mrefu kufuatia kujiweka kando kujishughulisha na Chadema kutokana na na chama hicho kumpokea Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa na kumpitisha kugombea nafasi ya urais akiviwakilisha vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ajitokeza hadharani na kutoa msimamo wake wa kustaafu siasa, huku akimtuhumu mgombea huyo kuwa alihusika moja kwa moja na sakata la Richmond, jambo ambalo limezua mjadala mkubwa kwa jamii.
Mkufunzi Msaidizi kutoka Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma (SJMC) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Godlisten Malisa, alipotakiwa na Nipashe kutoa maoni yake, alisema pamoja na kukubaliana na hotuba ya Dk. Slaa, lakini haikutolewa katika muda muafaka.
“Dk. Slaa ni kiongozi anayeheshimika kutokana na mchango wake mkubwa wa kuuimarisha upinzani na hasa Chadema, lakini alichokisema na hasa dhidi ya Lowassa kilipaswa kusemwa wakati wa mchakato wa kumpokea Chadema ama kabla ya kuingia kwenye kipindi cha kampeni,” alisema.
Malisa alisema, alipaswa kusema kabla, ili kuwasaidia watu ambao tayari wameshaamua kuwa na Lowassa na pengine kumpigia kura kutokana na ushawishi wa kampeni zinazoendelea, na hivyo hotuba yake hiyo kutokuwa ya msaada sana kwa wakati huu.
Kwa upande wa Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Alexander Makulilo, alisema uamuzi alioufanya Dk. Slaa ni haki ya kidemokrasia ya mtu kama sheria za nchi zinavyoeleza.
“Alichokifanya ni haki ya kidemokrasia kwa kuwa katiba ya nchi imeeleza mtu halazimishwi kuwa chama fulani bali ni utashi wake,” alisema Dk. Makulilo.
Aidha, alisema kitendo hicho hakina haja ya kupingwa kwa kuwa watu wengi ni wafuasi na siyo wanachama.
Naye Mhadhiri Msaidizi wa Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es Salaam, Idara ya Mawasiliano, Danford Kitwana, alisema amesikitishwa na kitendo cha Dk. Slaa ambaye anaamimika kuwa na dhamira ya kulikomboa taifa na kuliletea mabadiliko baada ya kusema Chadema kimaadili kibaya kuliko chama tawala.
Kitwana alisema hana tatizo na mtazamo alioutoa Dk. Slaa, bali mashaka yanakuja kutokana na hotuba yake kuonyesha mafisadi wapo Chadema wakati inaaminika CCM ndicho chenye idadi kubwa ya mafisadi.
Profesa wa uchumi, ambaye pia ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe Tawi la Dar es Salaam, Prosper Ngowi, amesema kujiuzulu kwa Dk. Slaa kumetokana na upeo na mtazamo alionao kiongozi huyo katika kutazama mambo.
Prof. Ngowi alisema uamuzi wa kujiweka pembeni na siasa ya vyama au kushiriki ni hiari ya mtu hailazimishwi.