Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema kitamshitaki Balozi wa China nchini, Lu Younqing Umoja wa Mataifa (UN) kwa kukiuka Mkataba wa Vienna (Vienna Convention) wa mwaka 1964 ambao unaeleza uhusiano wa kibalozi kati ya nchi na nchi.
Aidha, kimesema kitaiandikia barua Serikali ya China ili kutaka ufafanuzi kama imemtuma Balozi wake kufanya kazi ya uenezi siasa kwenye vyama.
Tukio la Balozi huyo kuhudhuria mkutano wa hadhara wa CCM lilitokea Septemba tisa mwaka huu kwenye mkutano wa chama hicho uliofanyika Wilaya ya Kishapu Shinyanga, ambapo Katibu Mkuu wake, Abdulrahman Kinana alimtambushisha balozi huyo huku akiwa amevaa sare za chama hicho.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Waziri kivuli wa mambo ya nje ambaye pia ni Mbunge wa Nyamagana Jijini Mwanza, Ezekiel Wenje alisema Chadema wameamua kuchukua hatua hizo ili kukomesha vyama vya siasa kutumia mabalozi kama wawakilishi wa vyama vyao kwa kufanya uenezi kwenye mikutano ya siasa.
Wakati Wenje akisema hayo Katibu Mkuu Taifa wa Chadema, Dk Willibrod Slaa amesema chama chake kinaangalia namna ya kumchukulia hatua za kumshtaki Balozi huyo akidai kuwa kitendo cha kushiriki siasa za CCM na kisha kuvalishwa kofia ya chama hicho ni kiunyume na taratibu za UN.
Kauli ya Dk Slaa aliitoa juzi jioni wakati akiwahutubia wakazi wa Jiji la Mbeya na vitongoji vyake kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Viwanja vya Ruanda Nzovwe.
Kiongozi huyo yupo mkoani Mbeya akiwa ameambata na Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ akifanya mikutano maeneo mbalimbali lengo likiwa kuwaeleza wananchi wa Mbeya kuhusiana na kitendo kilichomtokea Sugu na wabunge wengine bungeni hivi karibuni.
Kwa mujibu wa Dk Slaa, balozi huyo alikiuka sheria na taratibu za Umoja wa Mataifa kwa kitendo chake ambapo alionekana kupanda kwenye jukwaa la mkutano wa CCM na kuvalishwa kofia ya chama hicho.
Kwa upande wake, Wenje alidai kuwa kwa mujibu wa mkataba wa Vienna Convention wa mwaka 1964 ambao unaeleza mahusiano ya kibalozi unakataza mabalozi kujingiza kwenye mambo ya ndani ya nchi ikiwa pamoja na kushiriki kwenye siasa.
“Mkataba wa Vienna Convention wa mwaka 1964 Ibara ya 41 kifungu kidogo cha kwanza kinakataza mabalozi kujiingiza kwenye mambo ya ndani ya nchi ikiwa pamoja na kufanya siasa.” alisema Wenje na kuongeza;
“Kitendo alicho kifanya balozi wa China kufanya kazi ya uenezi wa chama kimevunja mkataba huo jambo ambalo hatuwezi kulivumilia hata kidogo,”alisema.
Alifafanua kuwa licha ya Ibara hiyo kukataza jambo hilo Ibara ya 3 ya mkataba huo inataja wazi kazi wanazotakiwa kufanya balozi pindi anapokwenda kuwakilisha nchi yake sehemu nyingine.”alisema.
Source: Mwananchi