Raia wa Nigeria aliyefukuzwa Kenya miezi minne iliyopita kwa kuhusishwa na biashara ya dawa za kulevya, amekamatwa tena nchini humo akiwa na pakiti 425 za heroin, akiaminika kwamba alipitia Tanzania.
Mtu huyo aliyetajwa kwa jina la Enobemhe Emmanuel Peter inaaminika alishukia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam, akitokea Nigeria na kisha kwenda Kenya kwa barabara, kupitia mpaka wa Namanga mkoani Arusha.
Peter alikamatwa pamoja na mwanamke ambaye ni raia wa Kenya, usiku wa Ijumaa iliyopita jijini Nairobi na anatarajiwa kufikishwa mahakamani leo.
Raia huyo wa Nigeria ni kati ya wageni waliofukuzwa nchini humo Juni mwaka huu kwa agizo la Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta aliyeamuru raia wa kigeni wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya wafukuzwe nchini humo.
Mkuu wa Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya cha Kenya, Dk Hamisi Massa alisema uchunguzi zaidi wa dawa hizo utafanyika kabla mtuhumiwa huyo kufikishwa mahakamani.
“Ni kati ya watu waliokuwa wamefukuzwa nchini katika nyumba aliyokamatiwa kulikutwa pia na pakiti 425 za heroin,” alisema Dk Massa.
Mtu huyo amekamatwa kutokana na kuwapo kwa taarifa zilizoonyesha kuwa, watu wengi waliofukuzwa Kenya kutokana na kujihusisha na biashara hiyo sasa wamerejea tena.
Julai 9 mwaka huu, Ofisa Uhamiaji wa nchi hiyo, Edward Kabiu Njau alifikishwa mahakamani na kushtakiwa kwa kumruhusu Anaeke Chimenze, aliyefukuzwa nchini humo, kurejea tena.
Chimenze ambaye ni raia wa Nigeria mwenye pasi ya kusafiria namba 02743350, pia anadaiwa kurudi nchini humo kupitia mpaka wa Namanga.
Uhamiaji Tanzania
Msemaji Mkuu wa Idara ya Uhamiaji, Naibu Kamishna, Abbas Irovya alisema hawezi kuzungumzia suala hilo kwa kuwa yupo nje ya ofisi. “Mtafute Tatu ndiye mtu wa habari zaidi, kama atakuwa amepata hizo taarifa atakueleza,” alisema.
Mwananchi ilipomtafuta Tatu Iddi alisema hajapata taarifa hizo na kutaka mwandishi amtumie barua pepe ikiwa na maelezo ya mtu huyo aliyekamatwa ili aweze kutafuta taarifa zaidi.
Source: Mwananchi