Blogger Widgets

Monday, April 28, 2014

Uliskia hii?? Mashamba ya aliyekuwa gavana wa BOT, Daudi Balali kugawanywa kwa wananchi..!!

 Aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), marehemu Daudi Balali.
Kilombero. Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero imeamua kufuta miliki ya mashamba yote makubwa yasiyoendelezwa na taratibu mpya zinafanyika ili kuyamilikisha kwa wananchi.

Kati ya mashamba hayo, matatu ni ya aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), marehemu Daudi Balali na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Klabu ya Simba, Marehemu Priva Mtema yaliyoko katika vijiji vya Lungungole na Merera ambayo wananchi wameshayavamia na kuendeleza shughuli za kilimo.

Akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Kilombero juzi, Mwenyekiti wake, David Ligazio alisema taratibu za kuomba hatimiliki za mashamba hayo zifutwe zinaendelea.

Ligazio alisema wamiliki wa mashamba hayo wameshapewa notisi na orodha yao imeshawasilishwa kwa Kamishna wa Ardhi ili aridhie kufutwa kwa hati za mashamba hayo.

Alisema uamuzi wa kuyataifisha umekuja baada ya halmashauri kubaini kuwa yamekuwa hayaendelezwi na hivyo kusababisha maeneo hayo kuwa misitu wakati wananchi wanahitaji maeneo ya kulima.

Alisema ukaguzi wa kumbukumbu umeonyesha kuwa idadi kubwa ya wamiliki hao hawapo wilayani Kilombero na maeneo hayo yanamilikiwa kwa hati za muda mrefu bila kufuata taratibu.

Alisema utaratibu unaofanyika sasa ni kuwaagiza watendaji na wenyeviti wa vijiji, kuanisha ukubwa halisi wa mashamba hayo ili kurahisisha kazi ya kuyagawa kwa wananchi katika siku zijazo.

Akizungumzia hatua hiyo, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka alisema taarifa hiyo haijafika ofisini kwake, lakini akabainisha kuwa kuna watu wengi wanaomiliki ardhi kubwa mkoani Morogoro bila kuwa na hatimiliki wala kufuata taratibu huku wakiwa wanawatisha wananchi.

Aliwataka wananchi hao kujisimamia, waondoe unyonge na kuzingatia taratibu za ardhi, kwamba inatakiwa kugawiwa kupitia mkutano mkuu wa kijiji, vinginevyo wana haki ya kujitwalia maeneo hayo na kufanya maendeleo mengine.

“Kuna matukio unakuta mtu anakaa na mwenyekiti wa kijiji na kujifungia, wanajadili wenyewe na kugawiana maeneo ya kijiji bila kuwashirikisha wananchi, hawa wananchi wanatakiwa kukataa hali hiyo,” alisema.

Maeneo yanayogawiwa

Mwenyekiti wa halmashauri aliyataja maeneo mashamba yanayotakiwa kugawanywa kwa wananchi na ukubwa wake katika mabano kuwa ni Lungongole (ekari 375) na Merea (ekari 373). Pia kuna shamba lenye ukubwa wa hekta 887 linalomilikiwa na Balali, ekari 491 zinazomilikiwa na George Teni katika Kijiji cha Kisegese na ekari 500 zinazomilikiwa na Aloyce Lyenga katika Kijiji cha Idete.
Katika orodha hiyo pia kuna ekari 30,000 za Kampuni ya Merera Plantation Ltd katika Kijiji cha Merera.

Mashamba mengine ni ekari 102 za Abdallah Sajiri zilizopo Kining’ina, ekari 295 za Peter Warwic zilizopo Lumemo, ekari 484.9 za Sadru Meghji zilizopo Msolwa Ujamaa, ekari 120 za Ranifa EC &DEV. Group zilizopo Kisegese na hekta 5,128 za Rubada zilizopo Ngalimila.
Ligazio alitaja mashamba mengine kuwa ni ekari 2,390 za kampuni iliyokuwa ya usafirishaji mkoani Morogoro zilizopo Mbingu, ekari 875 za Jerome Mwakifuna zilizopo Idete, ekari 656 za Priva Mtemanyanja zilizopo Lungongole na ekari 1,500 za Ngwasi River Valley Inv. zilizopo Mlimba.

Source >>Mwananchi<<