Blogger Widgets

Friday, October 11, 2013

SPORTS: Rooney afunguka kuhusu Ferguson!!!

Manchester, England. Kitendo cha kocha wa zamani wa Manchester United, Alex Ferguson kumhamisha nafasi anayocheza uwanjani Wayne Rooney kilitaka kusababisha nyota huyo kutaka kuihama klabu hiyo msimu uliopita, lakini uongozi wa klabu hiyo ulikataa kumuuza.
“Kila mtu katika klabu yetu anajua nafasi ninayotaka kucheza, kitendo cha kocha Ferguson kunichezesha nafasi tofauti kiliniudhi, kocha alikuwa akitaka nicheze nafasi ya kiungo, mimi sikutaka kucheza nafasi hiyo,”alisema Rooney.


Alisema “Ni kweli katika mechi nilizocheza nafasi ya kiungo nilicheza vizuri, lakini ni wazi nilikuwa sitaki kucheza nafasi hiyo, kwa hiyo nilimwambia kocha nataka kucheza nafasi ninayostahili kucheza ambayo ni nafasi ya ushambuliaji, lakini kocha akawa hataki.”
Rooney anasema,”Nafikiri jambo kama hilo kisaikolojia lazima litakuathiri, mimi liliniathiri katika baadhi ya mechi, najua msimu uliopita haukuwa mzuri, lakini sababu kubwa ni kwamba katika mechi nyingi kocha alikuwa hanipangi katika nafasi niliyokuwa nastahili kucheza.” Ingawa Rooney ameongelea sababu hizo zilizosababisha akose furaha katika klabu ya Manchester United msimu uliopita, anasema hakuwa na tatizo na klabu hiyo katika kipindi cha usajili msimu huu.
“Kwa kweli katika kipindi chote cha usajili msimu huu  nilikuwa nimetulia na kufurahia maisha, mke na mimi tulikuwa tumepata mtoto mwingine,” alisema Rooney.
Alisema,”Msimu huu nimefanya kazi kwa bidii katika klabu ya Mancheter United, niliumia kwa sababu ya kufanya kazi kwa bidii, nina mtazamo mzuri na nataka kuwathibitishia watu kwamba mimi ni mchezaji wa kiwango cha juu.”
Wakati wa kipindi cha usajili msimu huu, klabu ya Manchester United ilikataa mara mbili ofa ya Chelsea kutaka kumsajili Rooney, ambapo mchezaji huyo katika kipindi chote hicho alikaa kimya katika kulizungumzia suala hilo.
“Nilikaa kimya na kuacha kulizungumzia suala hilo kwa sababu nilikuwa nikijua klabu itatoa msimamo wake na ndivyo ilivyofanya kwani ilikataa ofa za klabu zilizokuwa zikinitaka,”alisema Rooney.
Alisema,”mimi nilizungumza na viongozi wa klabu na kuwaachia suala hilo, sikulizungumzia suala hilo kwenye vyombo vya habari kwa sababu nilitaka kutulia na kuweka mtazamo wangu katika soka.”